Alhamisi, 22 Mei 2014

KILIMO BORA CHA ZAO LA NYANYA.

SOMO LA KWANZA KILIMO BORA CHA ZAO LA NYANYA
I. MUHTASARI.
Nyanya ni mojawapo ya mazao makuu ya kilimo cha mbogamboga ulimwenguni na hushika nafasi ya 2 baada ya viazi mbatata. Hapa nchini Tanzania nyanya hulimwa kwa wingi karibu mikoa yote hususani mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro, Iringa, Mwanza, Dodoma, Pwani na mbeya.

LISHE.
Matunda ya nyanya zilizoiva hutupatia:- § Vitamini A,B na C § Madini aina ya chokaa. § Maji - 94% § Utomwili(Protini )– 1% § Mafuta – 0.1% § Wanga – 4.3% § Nyuzi nyuzi (Fibres) – 0.6%

MATUMIZI.
Nyanya hutumika kama:- § Kiungo cha kupukia. § Huliwa ikiwa mbichi kama kachumbari. § ………………………………………………………………… …... § ………………………………………………………………… …… § ………………………………………………………………… …..
CHANZO CHA ZAO LA NYANYA.
Mmea wa nyanya uligundulika huko Amerika ya kati na kusini, baadaye ukaenea katika mabara mengine, ulizalishwa huko Mexico na kuletwa hadi Ulaya na baadaye ukasambaahadi kwenye nchi za tropiki.

II. MAZINGIRA.
Nyanya hustawi katika udongo wa aina nyingi ili mradi uwe na wepesi na usiotuamisha maji. (PH 5 – 7) Hali ya unyevu na joto jingi la usiku huleta majani mengi na matunda machache. Joto ni kati ya 18oC -30oC.Vilevile joto jingi, mwanga kidogo pamoja na hali ya unyevunyevu husababisha:- § Magonjwa mengi kuenea. § Mmea kuwa na majani mengi. § Matunda madogo ambayo huchelewa kukomaa. Zao ili hupendelea mvua za wastani pamoja na kipindi kirefu cha jua.Hali ya mvua nyingi pamoja na baridi kali husababisha kuenea kwa magonjwa na wadudu waharibifu.Hii ndio sababu nyanya zinazozalishwa kwa kilimo cha umwagiliaji huwa na mavuno mengi yenye ubora kuliko wakati wa mvua.

III. AINA ZA NYANYA.
 Zipo aina za nyanya zinazolimwa hapa nchini zinazofahamika na wakulima wengi ambazo hutoa mavuno mengi na bora, zinazostahimili magonjwa, zinazokomaa mapema na zenye ladha nzuri, umbo la kuvutia. Aina hizo zimegawanyika katika makundi makuu mawili kutegemea ukuaji wake. Aina fupi: Roma, Dwarf germ, ……………………………………………….. Aina ndefu:-Moneymaker, ………………………………………………………..

IV. KUSIA MBEGU. 
Mbegu za nyanya huoteshwa kwanza kwenye kitalu na baadaye huhamishiwa shambani.Matayarisho ya kitalu hufanyika wiki 1 au 2 kabla ya kusia mbegu. Tengeneza tuta lenye upana wa mita 1 na urefu wa kuanzia mita 5 hadi urefu unaoweza kuhudumia kwa urahisi. Vunja mabonge makubwa kwa kutumia jembena kulainisha udongo vizuri.Changanya mbolea za asili zilizooza vizuri kama vile Samadi au mboji kiasi cha debe 1- 2 katika eneo la mita mraba 1. Sawazisha kwa kutumia reki au kifaa kingine. Mwagilia kitalu siku moja kabla ya kusia, kisha sia mbegu katika mistari yenye nafasi ya sentimita 10 – 15 kutoka mstari hadi mstari. Kiasi kinachotosha eneo la mita mraba 1 ni gramu 3 – 5 (sawa na nusu kijiko cha chai hadi kimoja) Kiasi hiki cha mbegu huweza kutoa miche inayoweza kutosha kupandikiza katika eneo la mita mraba 100. Kiasi cha mbegu kinachohitajika kwa hekta 1 ni gramu 300. Weka matandazo kama vile nyasi kavu na kasha mwagilia maji asubuhi na jioni mpaka mbegu zitakapoota.Mbegu huota baada ya siku 5 – 10. Ondoa matandazo baada ya mbegu kuota na endelea kumwagilia maji hadi miche itakapofikia kupandikizwa.Jenga kichanja ili kzuia jua kali na matone ya mvua yasiweze kuharibu miche michanga.

V. KUTAYARISHA SHAMBA.
 Matayarisho ya shamba kwa ajili ya kupandikiza miche ya nyanya yaanze mwezi 1 kabla.Katua ardhi katika kina cha kutosha hadi kufikia sentimita 30. Lainisha udongo kwa kuvunja mabonge makubwa kwa kutumia jembe. Weka mbolea ya asili wiki 2 kabla ya kupandikiza. Tani 20 kwa hekta 1 (sawa na ndoo 1 – 2) kwa mita ya mraba.Hii ni muhimu sana kwani zao la nyanya huhitaji chakula kingi toka kwenye udongo.(heavy feeders).

VI. KUPANDIKIZA.
 Upandikizaji wa miche shambani hufanyika baada ya wiki 4 – 6 tangu kusia mbegu kitaluni na hutegemea hali ya hewa.Siku ya 10 – 14 za mwisho kwenye kitalu izoeshe miche hali halisi ya shambani.(hardening off). Wakati huu ipatie miche maji na ondoa kivuli. Mwagilia maji kwenye kitalu kabla ili kurahisisha ungoaji wa miche na kuepuka kukata mizizi. Pia ni muhimu kumwagilia shamba siku moja kabla ya kupandikiza. Iwapo mbolea za asili hazikutumika wakati wa kutayarisha shamba unashauriwa kuweka mbolea ya mchanganyiko (NPK 5.10.5) kiasi cha gramu 5 kwa shimo wakati wa kupandikiza.Baada ya kungoa miche kitaluni usichelewe kuipandikiza, pandikiza muda wa asubuhi sana au jioni ili kuepuka jua kali linaloweza kunyausha miche. Wakati wa kupandikiza hakikisha mizizi haipigwi na jua kwa kuiweka kwenye ndoo au chombo chochote chenye udongo wa unyevunyevu. Pandikiza miche katika kina cha sentimita 2 – 3 zaidi ya ilivyokuwa kwenye kitalu, hii husaidia:- § Kupata mizizi mingi mipya. § Kunyonya viini lishe. § Miche kukua kwa nguvu zaidi. NAFASI: Nafasi zinazotakiwa kutumika kwenye miche shambani hutegemea na:- § Aina ya nyanya. § Kama mimea ya nyanya itawekewa miti. § Kama itaondolewa machipukizi. § Rutuba iliyoko kwenye udongo. Aina fupi ya nyanya: hupandikizwa katika nafasi ya sentimita 90 x 50 kutoka mstari hadi mstari na sentimita 50 toka mche hadi mche. Nafasi kati ya tuta ni sentimita 60. Aina hii haihitaji kuegeshwa miti. Aina ndefu inayohitaji kuegeshwa kwenye miti hupandikizwa katika nafasi zifuatazo:-sentimita 75 mstari hadi mstari na sentimita 50 – 60 toka mche hadi mche.

VII. KUTUNZA SHAMBA
 § Kuweka matandazo. Baada ya kuhamisha miche shambani weka matandazo ili kuhifadhi unyevu na kuzuia magugu. Pia husaidia mmomonyoko wa udongo na kutunza rutuba, pia hupunguza udongo kurukia kwenye matunda na kuyaacha katika hali ya usafi. Nyanya zenye matandazo huzaa matunda yaliyo bora zaidi. § Kusimika miti ya kuegesha mimea ya nyanya. Wiki 2 baada ya kupandikiza simika miti ya kuegeshea nyanya, miti ni muhimu iwe imara na isiyooza wala kuanza kuota.Simika miti kiasi cha sentimita 8 – 10 toka kwenye sina la mmea. Mti usimikwe upande wa nje wa mstari ili kuzuia kuumiza mimea wakati wa kuhudumia.Kisha ushindilie mti sentimita 20 – 50 kwenda chini ya ardhi.Mti uwe na urefu wa mita 1.5 – 2 na unene wa sentimita 2 – 3. § Kufunga nyanya kwenye miti. Aina ndefu ya nyanya ni lazima ifungiwe kwenye mti ili:- § Kuzuia mmea usitambae chini. § Kurahisisha unyunyuziaji wa dawa. § Umwagiliaji wa maji. § Uchumaji matunda. Muhimu: Wakati wa kufunga kamba, isiwe imekazwa sana na wala isiwe imelegea kupita kiasi. Kamba ifungwe umbo la nane kati yam mea na mti.Kamba ya katani au ya mgomba huweza kutumika. Funga kamba chini ya jani kila baada ya sentimita 20 – 25. § Kuondoa machipukizi: Kwa aina ndefu ya nyanya ni muhimu kuondoa machipukizi kila mara baada ya wiki 1. Muda mzuri ni asubuhi.Ondoa machipukizi yote na acha shina 2 tu. Usitumie kisu au mkasi bali vunja kwa mkono ili kuepuka kueneza magonjwa ya virusi na bacteria. Sababu za kuondoa machipukizi: - Huchukua chakula cha mmea. - Mmea hutoa matunda mengi madogo ambayo hayafai kwenye soko. § Kuondoa Majani: Ondoa majani yote yanayoonyesha dalili zote za magonjwa au kushambuliwa na wadudu, yale yote yaliyozeeka ili kupunguza hali ya unyevu na kuruhusu hewa ya kutosha kwa mimea. Majani yote yaliyoondolewa yachomwe moto ili kuliweka shamba katika hali ya usafi. § Kukata kilele: Kwa kawaida aina ndefu ya nyanya huzaa ngazi 6 – 8 za matunda lakini mmea una uwezo wa kubeba ngazi 5 – 6. Hivyo ni muhimu kukata sehemu ya juu yam mea (kilele) ili kusimamisha ukuaji wake. Hii husaidia chakula kingi kwenda kwenye ngazi chache na hivyo kupata matunda makubwa. Kata kilele wakati mimea ifikiapo ngazi ya 6 na usikate karibu sana na ngazi na kata mkato wa mlalo ili kuruhusu maji kutiririka. Hata hivyo kama udongo una rutuba nyingi sana unaweza kuachia hata ngazi 8. § Palizi: Palilia mara kwa mara kwa kupandishia udongo kwenye shina kwa uangalifu ili kuepuka kukata mizizi. Palizi husaidia maji na hewa kupenya kwa urahisi kwenye udongo. Hata hivyo kama mimea imewekewa matandazo ya kutosha na haina miti ya kuegeshea ni vyema palizi ikaachwa ili kuepuka kuumiza matunda. § Kumwagilia maji: Kwa kawaida nyanya hutoa mazao mengi wakati wa kiangazi kuliko wakati wa mvua za masika.Mwagilia maji ya kutosha mara 2 kwa siku hasa wakati matunda ya kwanza yanapoanza kutunga. Kumwagilia maji mengi kupita kiasi au kidogo sana husababisha matunda yawe na hitilafu ya kupasuka. § Kuweka mbolea ya kukuziatop dressing). Mbolea zenye nitrogeni ndio hutumika kwa kukuzia,mfano S/A,UREA au CAN na hutumika wiki 2 – 4 tangu kupandikiza miche kwani inakuwa tayari na mizizi mipya itakayonyonya mbolea hiyo. Mbolea hii ya kukuzia huwekwa mara 2. Mara ya kwanza weak gramu 5 kwa kila mmea za SA au CAN. Rudia tena wakati inaanza kutoa matunda. Muhimu: Kiwango cha nitrogeni kinatakiwa kidhibitiwa na kurekebishwa ili kitumike kiasi kile tu kinachohitajika vinginevyo mimea itakuwa na majani mengi sana yenye afya bila matunda na itachelewa kukomaa na kuiva kwa matunda.

VIII. MAGONJWA: 
Nyanya ni zao ambalo hushambuliwa sana na magonjwa mbalimbali. § Magonjwa ya ukungu (Early blight): Ambukizo:- Fungusi aitwae Altenaria solani. Dalili: Majani: Kingo za majani huwa na madoa ya rangi nyeusi iliyochanganyika na kahawia, pembe zake huwa za njano. Shina: Huwa na madoa kama ya kwenye majani lakini makubwa na kusambaa zaidi.Baadaye madoa hupanuka na kuwa mabaka makubwa ya rangi nyeusi, makavu na yaliyodidimia,shina huwa jembamba, usawa wa ardhi na hudumaa na huvunjika kwa urahisi. Matunda: Huwa na madoa meusi ya mviringo yenye umbo la yai.Madoa huonekana zaidi kwenye kikonyo cha tunda na kwenye sehemu iliyopasuka. Kadri tunda linavyozidi kuiva madoa haya huongezeka zaidi. § Bakajani (late blight) Ambukizo: Phytophthora Infestans. Dalili za ugonjwa huu huanza kuonekana kwenye jani la chini. Majani na shina huwa na mabaka makubwa yenye rangi nyeusi au kahawia nzito. Katika hali ya unyevunyevu, majani huoza na hatimaye uyoga mweupe huonekana chini ya jani. Baadaye majani huakuaka na kuwa yameunguzwa na moto. Matunda yaliyopatwa na ugonjwa huu huwa madoa ya rangi ya kijani iliyochanganyikana na kahawia. Baadaye huwa makubwa na kuoza, ukipasua tunda lilooza utaona weusi. Nyanya zenye ugonjwa huu zikihifadhiwa kwenye sehemu zenye unyevunyevu, hutoa uyoga mweupe. Jinsi unavyoambukizwa na kuenea:- Ukungu wa ugonjwa huu hutokea kwenye majani ama shina huambukizwakutoka mmea hadi mmea kwa njia ya upepo, mvua na umwagiliaji wa majai ya mashambani. Kuzuia Ugonjwa wa Bakajani:- - Kubadilisha mazao, usipande nyanya katika eneo moja mfululizo. - Kuweka matandazo shambani - Kupunguzia matawi na kuondoa majani yaliyoshambuliwa. - Kung’oa masalia yote shambani mara baada ya kuvuna na kuchoma moto. - Sia mbegu katika kitalu kilichotayarishwa vizuri. - Tumia mbegu bora ambazo hazijashambuliwa na ugonjwa. - Otesha aina ya nyanya zinazovumilia mashambulizi ya ugonjwa huu. - Tumia dawa za ukungu kama vile Dithane M-45, Ridomil, Tposin M70, Copper Oxichloride (Cipro), Cupric Hydroxide, (Champion) § Mnyauko Bakteria:- (Bacteria Wilt) Ambukizo:- Pseudomonas Solanacerium Mmea ulioshambuliwa hunyauka ghafla bila kuwa njano hasa wakati wa jua kali na njano. Baadaye mmea hudumaa majani na vikonyo vyake hukunjamana, shina likikatwa karibu na usawa wa ardhi rangi ya kahawia nzito huonekana kwenye sehemu ya kusafirishia maji. Sehemu iliyokatwa ikiwekwa kwenye maji uji mzito kama maziwa huchuruzika. Jinsi ugonjwa unavyoambukizwa na kuenea:- Ugonjwa huu huwa katika udongo na kujitokeza zaidi wakati wa joto na pale ardhi ikiwa na unyevenyevu. Huweza kuishi ardhini muda mrefu katika masalia ya mimea ya nyanya na kushambulia mimea mingine. Ugonjwa ukishakuwepo ardhini huenea haraka kwa njia ya umwagiliaji maji na maji ya mvua kufuata mteremko wa ardhi. Pia huenezwa toka mmea hadi mmea kwanjia ya mizizi kugusana. Kuzuia ugonjwa:- - Otesha mbegu kwenye kitalu ambacho hakina ugonjwa huu. - Epuka kupanda nyanya kwenye sehemu ambayo ina ugonjwa huu. - Badilisha mazao shambani - Otesha nyanya zinazostahimili ugonjwa huu. - Ng’oa na choma moto mimea yote iliyoathirika na usipande tena nyanya au jamii yake kwa kipindi cha miaka 4- 5. § Mnyauko Fuzari ( Fuzarium Wilt) Ni ugonjwa wa ukungu. Husababisha majani kuwa rangi ya njano na mimea kunyauka hasa wakati wa jua kali, majani yaliyoshambuliwa huvunjika kwa urahisi. Kama shina likinyofolewa karibu na usawa wa ardhi rangi ya kahawia huonekana. Mmea: Hunyauka ----- huwa njano --- hufa. Kuzuia ugonjwa: - Kung’oa mimea iliyoshambuliwa na kuichoma moto. - Otesha aina ya nyanya zenye ukinzani kama vila Roma, VFM, n.k. - Tumia dawa kama vile Topsin M70, dawa inyunyiziwe kwenye udongo. § Batobato (Tomato Mosaic Virus) Husababishwa na virusi. Hushambulia majani machanga na yaliyozeeka. Majani yaliyoshambuliwa hukunjamana na kudondoka. Hali kadhalika majani yaliyozeeka huvunjika kwa urahisi na huwa na rangi nyeusi, kijivu au kikahawia china ya jani. Mwisho majani kuhakauka na kufa. Zuia ugonjwa kwa yafuatayo:- - Epuka kuotesha nyanya kwenye eneo lililoathirika - Ng’oana choma moto mimea yote iliyoshambuliwa. - Otesha mbegu zilizodhibitishwa kitaalamu - Epuka kuhudumia mimea mingine baada ya kuhudumia ile iliyoathirika. osha mikono kabla ya kuhudumia mingine. - Safisha vifaa vyote kama vile visu, mikasi kwa maji na sabuni baada ya kuvitumia. - Usivute sigara ndani ya shamba la nyanya. - Otesha aina ya nyanya zinazostahimili magonjwa ya batobato. § Ugonjwa wa madoa jani (Septoria leaf spot) Husababishwa na ukungu na kushambulia majani na kuwa na madoa meusi na kingo zake huwa na rangi ya kijivu iliyoambatana na madoa meusi. Kuzuia:- - Nyunyiza dawa za ukungu kama vile Dithane M45, Blitox na Coper fungicides. § Scleretonia Rot: Ambukizo: Ni mdudu aina ya fungusi aitwaye sleratinia scerotirum. Dalili za ugonjwa:- Muozo mwepesi katika shina ikifuatiwa na unyaukaji wa ncha za mmea na matawi. Wakati wa unyevunyevu, viini vyeupe vya fungusi hutokea katika sehemu zilizoshambuliwa na ugonjwa. Viini vikubwa vya ugonjwa vigumu na vyenye rangi nyeusi huwepo ndani ya mmea ulioshambuliwa na kisha mmea mzima hunyauka na kufa au hukauka. Jinsi unavyoambukiza na kuenea: Fungusi wa ugonjwa wana uwezo wa kuishi ardhini kwa muda mrefu. Nyakati za baridi na unyevunyevu wale waliokuwa usawa wa ardhi huzaana kwa wingi na kisha kupeperushwa na upepo. Ugonjwa unaambukizwa pale ambapo maua makavu na majani yenye ugonjwa yakigusana na sehemu za mimea isiyo naugonjwa. Ugonjwa huu hutokea zaidi wakati wa mvua, baridi na nyakati za ukungu na umwagiliaji ndipo ugonjwa huenea zaidi. Mimea mingi ilimwayo na majani hushambuliwa sana na ugonjwa huu. Kuzuia:- - Tumia dawa za aina ya fungicide. - Epuka kupanda mimea katika eneo lililoshambuliwa sana na ugonjwa hasa wakati wa baridi.

HITILAFU ZA MATUNDA
 Kupasuka matunda: Kuna aina mbili za mipasuko; mpasuko wa mviringo na mpasuko wa nyota. Mpasuko wa mviringo: Hutokea wakati mmea haukupata maji ya kutosha hasa wakati wa jua kali. Wakati huu maji yaliyoko kwenye tunda hayawezi kulingana na maji yanayopotea angani kama mvuke. Mpasuko wa umbo la nyota: Hutokea hasa tunda linapokuwa na maji mengi na wakati huo unyevu angani ni mwingi sana. Hivyo tunda hushindwa kupoteza maji kwa njia ya mvuke na hupasuka kabla ya kukomaa. Hutokea zaidi kwenye nyanya aina ya Marglobe. Mpasuko wa mviringo na umbo la nyota huzuiwa kwa kumwagilia maji ya kutosha. § Kuoza kitako: Vidonda vyeusi vilivyodidimia huonekana kwenye kitako cha tunda. Sehemu hii baadaye hunyauka na ngozi huwa nyeusi. Hali hii hutokea zaidi wakati wa jua kali na katika sehemu zenye udongo wenye chumvichumvi na tindikali nyingi. Zuia hali hii kwa kuhakikisha udongo una unyevunyevu wa kutosha wakati wote. Pia epuka kuweka mbolea nyingi za chumvichumvi. § Mabaka ya matunda: Matunda yaliyopigwa na jua kali huwana mabaka hasa sehemu za ubavuni. Hali hii inaweza kuzuiwa kwa kuepuka kupunguza matawi mengi kwa wakati mmoja. § Matunda ya kijani kibichi: Mabega ya tunda huwa na kijani kibichi. Hitilafu hii hutokana na chanikiwiti kuwa nyingi na hutokea hasa wakati wa jua kali. Ili kuepuka hali hii unashauriwa kutoweka mbolea nyingi ya chumvichumvi na punguza mwanga wa jua kufunika matunda na majani makavu.

WADUDU WAHARIBIFU 
 Funza wa vitumba (AmericanBollworm) Ni funza watokanao na aina Fulani ya nondo. Wana rangi ya kijani hutokea baada ya mayai ya nondo kuanguliwa, kisha hutoboa matunda na kuishi humo. Jinsi wanavyokula na kukua husababisha matunda kuoza. Kuzuia:- Nyunyiza dawa za Carbarly, Dimethiote , Sumucidin na Dichlorvos. § Utitiri (Red spider mites) Ni wadudu wadogo sana na wenye rangi ya machungwa, nyekundu au kahawia. Vijidudu hivi hushambulia kwa kufyonza utomvu chini ya majani. Majani yaliyoshambuliwa huwa na rangi ya njano, hukunjamana, hukauka na hatimaye mmea hufa. Kuzuia:- Tumia dawa aina ya Morestan, Kelthane, Dimethoate, Diazinon, Ekalux, Poltrin na Profenofos. § Vidukari/wadudu mafuta (Aphids) Ni wadudu wadogo wenye rangi ya kijani, nyeusi au kahawia. Baadhi wana mabawa wengine hawana. Hufyonza utomvu wa majani na kusababisha mmea ulioshambuliwa kudhoofika, kudumaa, majani kunyauka na hatimaye kukauka. Kuzuia:- Tumia Dimecron, Actellic 50 Ec, Selecron, Sumicidin, Karate, Dichlorvos na Dimethoate. § Minyoo fundo: Wadudu wadogo weupe ambao hawaonekani kwa macho na huishi kwenye udongo. Hushambulia mizizi na kusababisha mimea kudhoofika na kushindwa kutoa matunda. Pia husababisha matunda kuiva kabla ya kukomaa. Uking’oa mmea ulioshambuliwa utaona mizizi ina vinundunundu. Kuzuia:- Tumia mzunguko wa mazao kwenye enneo moja. Baada ya kuvuna nyanya zao litakalofuata lisiwe la jamii ya nyanya, mfano Hoho, bilinganya. Kama madhara ni makubwa sana tumia dawa ya Furadan, na dawa za kufukiza ardhini kama Curaterr, Dazomet. Kumbuka:- Kumwagilia kwa kutumia mifereji kunaweza kusambaza minyoo shambani. tukutane tana wiki ijayo kwa somo la pili kwa maoni na ushauri usisite kuniandikia ua kutoa coment

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni