TANZANIA inakadiriwa kuwa na idadi ya kuku wa kienyeji wanaofugwa milioni 34.
Idadi hii ya kuku bado ni ndogo ikilinganishwa na mahitaji halisi ya Watanzania.
Ufugaji wa kuku ni nyenzo nzuri ya kujipatia kipato katika kaya kwa
sababu ufugaji huo hauhitaji mtaji mkubwa na hauna kazi kubwa
kiuendeshaji.
Katika ufugaji huria kuku hujitafutia chakula wenyewe, pia inapowezekana hupewa mabaki ya chakula, chenga,
pumba au nafaka yoyote inayopatikana katika mazingira husika.
Kwa walio wengi ifikapo nyakati za jioni, kuku hulala jikoni au ndani nyumbani kwa mfugaji mwenyewe.
Ufugaji huu ni rahisi kwa kuwa hauna gharama kubwa ila faida yake ni kitoweo tu au fedha kidogo sana.
Kutokana na lishe duni na kuzaana wenyewe kwa wenyewe (bila kubadili jogoo), kuku wa kienyeji walio wengi wana uzito mdogo.
Wana wastani wa uzito wa robo tatu za kilo hadi kilo moja wakiwa na umri wa zaidi ya mwaka mmoja.
Ila wakitunzwa vizuri zaidi na kuboreshwa wana uwezo wa kufikia uzito
wa kilo moja hadi moja na nusu katika umri wa miezi sita hadi nane.
Kwa upande wa utagaji wa mayai kuku 100 wa kienyeji kwa wastani hutaga
mayai 50 hadi 65 kwa siku. Wakitunzwa vizuri zaidi huweza kufikia
uzalishaji wa mayai 80 hadi 100 kwa siku.
Takriban wiki tatu zilizopita vijana wa Dar es Salaam walipata fursa
ya kuhudhuria semina ya Kamata Fursa Twenzetu iliyoandaliwa na Kampuni
ya Clouds Media Group ambapo lengo kuu lilikuwa ni kuwahamasisha vijana
wa Kitanzania kuchangamkia fursa zilizopo kwa ajili ya kujiongezea
kipato na kuepuka kubweteka kwa kusubiri ajira kutoka serikalini na
kwenye kampuni mbalimbali nchini.
Katika semina hiyo mwezeshaji aliyeonekana kuwa kivutio ni Yahaya
Nawanda ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida ambaye
alitoa mada ya faida ya kufuga kuku wa kienyeji.
Nawanda anasema alianza na kuku wawili ambao alipewa zawadi na
aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo kabla ya kuhamishwa kupelekwa mahali
pengine ambao walizaliana na kufikia kuku 32.
Mambo yanayomfanya mfugaji kuamua atumie njia fulani ya kufuga anasema
ni pamoja na uwezo wa kugharamia shughuli ya ufugaji wa kuku na ukubwa
wa eneo la kufugia.
Anasema baadaye idadi ya kuku iliongezeka na kufiki 2000 ambao hutaga
mayai 600 hadi 800 kwa siku ambapo baada ya kuuza hupata sh 240,000 kwa
siku moja.
Mbali ya hayo Nawanda anabainisha kuwa yai moja huuzwa kwa sh 300
ambapo kwa hesabu hiyo hupatia kiasi cha sh 7, 200,000 kwa mwezi.
Nawanda anasema bei ya kuku wa kienyeji kwa mfugaji anayeanza haizidi
sh 5,000 kwa maeneo ya mijini lakini kwa Singida vijijini ni sh 2000
lakini pia mahitaji yaliyopo sokoni hivi sasa ni makubwa kutokana na
jamii kutambua umuhimu wa kuku wa kienyeji kiafya.
Nawanda anasema ufugaji wa kuku wa kienyeji haumpasui mfugaji kichwa kwani huachwa wenyewe kujitafutia chakula na maji.
“Mara chache sana mfugaji huwapatia kuku chakula cha ziada ingawa kwa
ufugaji huu lazima kuwe na eneo kubwa la kutosha kuku kuzunguka na
kutafuta chakula,”anasema Nawanda.
Anasema kuku wa kienyeji ni rahisi ya kufugwa, gharama yake pia ni
ndogo, wanapata mazoezi ya kutosha na wanapata chakula mchanganyiko
kinachofaa kiafya lakini pia kikubwa ni kuingiza kipato.
Nawanda anasisitiza ufugaji wa kuku wa kienyeji katika wilaya yake na
kutamba kwamba ufugaji huo umeipatia maendeleo makubwa ikiwemo bima ya
afya.
Vilevile anasema ufugaji huo wa kuku wa kienyeji umesaidia kuondoa
tatizo la uhaba wa dawa katika zahanati na hospitali wilayani Iramba.
Mbali ya hayo Nawanda anasema hata katika sula la makazi bora wananchi
wake wamefanikiwa sana kwa sababu ya ufugaji wa kuku wa kienyeji.
“Leo hii ninajivunia kuwa mkuu wa Wilaya ya Iramba ambaye
nimefanikiwa kimaendeleo kupitia ufugaji wa kuku lakini pia kuna mkakati
wa kuanzisha kituo cha mafunzo kwa ajili ya ufugaji wa kuku na pia
napenda kusisitiza kwamba asiyetaka kufuga kuku ahame wilayani kwangu,”
anahitimisha Nawanda.
Mtaalamu wa kufuga kuku wa kienyeji Eva Kway mkazi wa Pugu nje
kidogo ya jiji la Dar es Salaam anasema ukiamua kufuga katika banda
utatakiwa kujenga banda lenye sifa zitakazokidhi mahitaji ya msingi ya
kuku.
Banda bora la kuku linatakiwa kuwa na jengo imara, pasiwe na sehemu
zilizo wazi kwenye msingi na kati ya ukuta na paa, banda lijengwe na
vifaa vinavyopatikana katika mazingira yako ili liwe na gharama
utakayoweza kumudu.
Vilevile unaweza kutumia matofali ya udongo, miti au fito.
Anasema jengo imara litazuia wezi, panya, vicheche, paka na nyoka kuingia ndani ya banda na kuwadhuru au kuiba kuku.
Anasema banda la kufugia kuku ni lazima liwe rahisi kusafisha hususani kuta na sakafu zisiribwe ili kusiwe na nyufa.
Mbali ya hayo Kway anasisitiza uimara wa jengo ni muhimu ili kudhibiti
wadudu wa kujificha katika nyufa kama papasi na viroboto.
“Sakafu ya banda lazima iwekewe matandazo kama pumba za mpunga,
maranda ya mbao, mabaki ya mazao au nyasi kavu kutegemeana na
kinachopatikana kwa urahisi katika mazingira yako,” anasema Kway
Anasema matandazo haya husaidia kunyonya unyevu unaotokana na kinyesi cha kuku au maji yanayomwagika katika banda.
Kway anasema banda hubakia kavu bila kuwa na harufu mbaya na wadudu kama inzi hata vimelea vya magonjwa hudhibitiwa.
Anasema eneo la nje kuzunguka banda ni lazima liwe na usafi wa kudumu
kuzuia wadudu kama siafu au mchwa wasipate upenyo wa kuingia ndani ya
banda.
Hasara
Kway anasema kuku huwa hatarini kuibiwa au kudhurika na wanyama wakali na hali mbaya ya hewa.
Ufugaji wa kuku wa kienyeji mbali ya kuwa na faida kubwa lakini ni hafifu, hufikia uzito wa kilo 1.2 baada ya mwaka.
Kuku hao pia huharibu mazingira kama kula mimea ya bustani, mazao kama nafaka na pia ni rahisi kuambukizwa magonjwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni